Wanasiasa kutoka eneo la Nyanza wametakiwa wawe wakizuru maeneo bunge yao kila juma ili kushinikiza wakazi wajiandikishe kama wapiga kura.
Huo ni wito wake mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti ya Kisumu Profesa Ayiecho Olweny, ambaye ametoa wito kwa wanasiasa kutenga muda wao katika juhudi za kuhakikisha kuwa wananchi wanajisajili kama wapiga kura ili wapate kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi mkuu ujao.
Ayiecho amesisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kushirikiana kwa pamoja kwa kuhakikisha kuwa wananchi ambao wametimiza umri wa miaka 18 wote wana vitambulisho vya kitaifa na wamesajiliwa kama wapiga kura.
"Tunatarajia wabunge na wawakilishi wadi kuchukua muda wa wiki moja katika maeneo yao ya uwakilishi kuchangia katika uhamasishaji wa kuchukua kura miongoni mwa wakaaz," alisema Olweny.
Kauli ya Olweny imeungwa mkono na mwenyekiti wa chama cha ODM eneo bunge la Kisumu ya Kati Seth Kanga ambaye pia amewataka wale ambao hawajajisajili kuhakisha kuwa wanasajiliwa mapema kabla ya muda uliowekwa kukamilika.