Huku wanasiasa wakiendelea kujiandaa na kampeni za uchaguzi mkuu ujao, watu wote wanaojishughulisha katika kuwania nafasi mbalimbali katika nyanja za siasa wametakiwa kujiepusha na matamshi ya chuki na kuwatenganisha watu.
Akiongea kwenye uga wa michezo wa shule ya msingi ya Jamvi La Wageni katika wilaya ya Likoni Kaunti ya Mombasa, mchungaji mkuu wa makanisa saba ya South Coast conference ya kiadventista Jonathan Mule, alisema kuwa wanasiasa ambao wanatafuta kuingia kwenye nafasi za kisiasa ifikapo mwaka wa 2017 sharti kuhubiri amani.
Mwanainjilisti huyo, ambaye aliongea mbele ya umati uliohudhuria hafla ya kufanya mchango wa kulijenga mojawapo ya makanisa ya dhehebu hilo alisema kuwa wanasiasa wengi hutumia muda wao mwingi kupiga siasa.
Hata hivyo, mchungaji huyo ambaye alionekana kuwa na msimamo na maadili ya uongozi wa kidini aliwataka wanasiasa amabo walishiriki kwenye hafla hiyo kutopiga siasa kanisani, na kuwaambia kuwa watatafutiwa muda ambao si siku ya kanisa kuja na kushiriki kwenye kuuza sera zao kwa wapiga kura kwenye eneo hilo.
Wanasiasa ambao walihudhuria waliheshimu wito huo na kupunguza siasa na kutoa michango yao kwa ajili ya ujenzi wa nyumba wa waumini wa kanisa la Kiadventista laJamvi.