Polisi katika kituo cha Bahati wilayani Nakuru kaskazini wanatafuta vijana watatu ambao wameingia mafichoni baada ya kudhulumu kiafya takriban vijana wanane katika eneo la Kirima, Engashura.
Peter Waigwa, Joseph Wokabi na Simon Nderitu, wote wa umri wa makamo, wanashukiwa kuwatesa vijana hao waliopashwa tohara mwaka jana, baada ya kuwalazimisha kuingia katika boma la kijana aliyepashwa tohara wiki tatu zilizopita.
Kulingana na mzee Mwangi Njui, watatu hao waliwalazimisha vijana hao kuvuta bangi 'waliposhindwa kujibu maswali'.
Aidha walilazimishwa pia kula majani yenye sumu pamoja na kuwekewa chai moto masikioni, kitendo kilichowafanya kulazwa kwenye hospitali kuu ya mkoa mjini Nakuru kwa takriban wiki moja unusu.
Madai hayo yamedhibitishwa na OCPD wa Nakuru kaskazini Duncan Nguthu, ambaye bila kutoa taarifa zaidi, alisema taarifa kuhusu dhulma hizo zimeandikishwa katika kituo cha polisi cha bahati.
Akiongea na mwandishi huyu kwa njia ya kipekee, Nguthu alisema amepoke malalamishi hayo, lakini kesi hiyo inaendelea kushuglkiwa.
“Nimepokea taarifa hizo, lakini si wajua kwamba si kila kitu ambacho hushugulikiwa na OCPD. Naomba uwasiliane na OCS ambaye aliwapa OB,” alisema afisa huyo.
Hata hivyo bwana Nguthu alisema lao kama idara ya polisi ni kuchunguza na kukamata washukiwa kwa usaidizi wa ripoti ya daktari.
Daktari aliyekuwa akiwahudumia vijana hao katika hospitali ya Nakuru Wambui Kinyajui, alidhibitisha kuruhusiwa kwa vijana hao kuondoka hospitalini, baada ya hali yao ya afya kuimarika.
Nguthu ametoa wito kwa wananchi kuwaripoti watatu hao watakapoonekana kwa uchunguzi zaidi.