Kina mama kutoka Wadi ya Gachuba, Eneo Bunge la Kitutu Masaba, wamehimizwa kukumbatia kilimo cha mboga na maua ili kuimarisha maisha yao.
Akizungumza katika Shule ya Msingi ya Bonyunyu, katika hafla ya kupeana mbegu kwa makundi ya kina mama, wakili Victor Swanya aliwasihi wakazi wa eneo hilo kukuza mboga kama njia mojawapo yakuimarisha maisha yao.
"Nawahimiza kina mama kukumbatia kilimo cha ukuzaji mboga kwa kuwa mashamba yanaendelea kupungua huku Gusii. Mboga hizi zitawapa pesa zinazoweza kuwasaidia pakubwa kuwasomesha watoto wenyu,” alisema Swanya.
Swanya vilevile aliwahimiza kina mama kujiunga katika makundi yakujiendeleza, huku akiwaomba viongozi wakisiasa kujitokeza kuwasaidia kina mama kifedha ili kuwawezesha kuanzisha miradi mbalimbali.
"Kina mama ni watu muhimu sana katika jamii na kwa kweli taifa haliwezi kuendelea bila yakuwepo kwa kina mama,” alisema Swanya.
Kwa upande wao, kina mama walionufaika kutokana na mbegu hizo za mboga walijitokeza kumshukru Swanya kwa usaidizi wake huku wakiipa serikali ya kaunti changamoto ya kuwatafutia soko la mazao yao.
"Tunamshukuru Swanya kwa kujitolea kutufadhili na mbegu hizi. Sasa ombi letu ni kwa Gavana Nyagarama kuhakikisha kwamba tumepata soko la kuuza mboga zetu kwa kuwa tutaanzisha mradi huu bila kusita," alisema Agnes Mokeira.