Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Msimamizi wa chama cha International Medical Scoop amesema kuwa akina mama 270,000 ulimwenguni hufariki kila mwaka kupitia ugonjwa wa saratani ya mfuko wa uzazi.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii, Meghan Kirng, alisema kuwa ugonjwa huo wa saratani ya mfuko wa uzazi ndio ugonjwa ambao umeonekana kuwaua akima mama kwa asilimia kubwa.

Katika Kaunti ya Kisii, asilimia 25 ya akina mama hupoteza maisha yao kupitia ugonjwa huo wa saratani ya mfuko wa uzazi kila mwaka.

Kulingana na Kirng, akina mama wanapaswa kutembelea hospitali kila wakati ili kupimwa ugonjwa wa saratani.

Alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha kupata matibabu mapema iwapo watapatikana na ugonjwa huo badala ya kuenda hospitalini baada ya ugonjwa huo kuenea mwilini.

Chama hicho kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Kisii kiliandaa kambi ya kuwapima akina mama ugonjwa huo wa saratani ya mfuko wa uzazi kwa wiki nzima katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii.

“Naomba akina mama kupimwa kila wakati kujua kama wameathirika na ugonjwa wa saratani ya mfuko wa uzazi na ule wa matiti ili kutibiwa mapema kabla ya kuenea mwilini,” alisema Kirng.

Gavana wa Kisii James Ongwae alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii pamoja na wadau wengine watajenga kituo cha kutoa matibabu ya ugonjwa wa saratani mjini Kisii kwa gharama ya shilingi bilioni mbili.