Wanawake katika Ukanda wa Pwani wameshinikizwa kujitosa katika siasa ili wawe na uwezo wa kufanya maamuzi muhimu kuhusiana na uongozi kupitia sheria bungeni.
Akiongea wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake ulimwenguni katika uwanja wa Tononoka mjini Mombasa siku ya Jumanne, mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa Mishi Mboko alisema kwamba Wanawake wana uwezo mkubwa wa kubadili uchumi wa taifa hili na uongozi hivyo basi wanapaswa kupigania nafasi za juu zaidi za uongozi.
Mboko alisema kwamba iwapo idadi ya wanawake itaongezeka bungeni basi Wanawake watakuwa na nafasi bora zaidi ya kupigania haki zao na jamii mashinani na pia kusukuma mabadiliko muhimu ya kiuongozi na mambo muhimu ya kulikuza taifa hili kiuchumi sawia na kuukabili umaskini.
"Tafadhali wanawake wakati umefika sasa ya nyinyi kujitokeza kwa wingi na kupigania nyadhfa mbalimbali za uongozi ili kubalisha uongozi na kukabiliana na umaskini wa taifa hili," alisema Mboko.
Kauli ya Mboko imeungwa mkono kikamilifu na Mwakilishi wa kike wa Kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa aliyewashinikiza Wanawake katika eneo la Pwani kuwa tayari kumenyana na wenzao wa kiume katika ulingo wa siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.
Katika maadhimisho hayo, Bi Mboko ameweka bayana kwamba atakiwania kiti cha ubunge cha Likoni huku mwezake wa Kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa akitangaza kuuwania ubunge wa Malindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.