Akina mama katika eneo la Shika Adabu kaunti ya Mombasa wametakiwa kujua hali yao ya afya kila mara kwa mujibu wa daktari anyesimamia afya ya akina mama walio wajawazito na ambao washajifungua.
Akizungumza katika hafla ya hivi majuzi ya uhamasisho kuhusiana na ugonjwa wa saratani mnamo siku ya Ijumaa wakati akina mama waliwapeleka wana wao kliniki, Sister Agatha alisema kuwa akina mama wengi hupuuza wanapotakiwa kuenda kliniki kupimwa ugonjwa wa saratani, ukimwi na vilevile kisukari hali ambayo amesema huchangia maafa ya akina mama wengi hasa wajawazito.
Daktari huyo pia alisema kuwa akina mama wengi huogopa unyanyapaa kutoka kwa jamii iwapo watapimwa na kupatikana kuwa wanaugua saratani ama ukimwi.
"Inavyofaa ni kuwa mama akijua ana mimba tayari afike katika kituo cha afya na kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kumwokoa mtoto ambaye hajazaliwa. Lakini takwimu za hospitalini humu zinasikitisha kwani wengi wao huwa hawajahudhuria japo mara moja na mara nyingi unakuta mama na mwanawe wanafariki au mmoja wao," alisema Agatha.
Aliongeza kusema kuwa saratani na maradhi mengine hupimwa mara kwa mara na sio siku maalum kama hiyo pekee yake na kuwahimiza wanawake na akina mama kujitahidi ili kuboresha maisha ya jamii na kuwahimiza akina mama hao kujitokeza kwa wingi na kuwafahamisha wasiojua.