Wakaazi kaunti ya Likoni wamelalamikia ukosefu wa bidhaa muhimu za soko zikiwemo nyanya, sukuma wiki miongoni mwa bidhaa zingine.
Akiongea na mwandishi huyu, Ali ambaye ni mchuuzi wa mboga eneo la kaunti hiyo amesema kuwa tokea sherehe za sikukuu za mwezi huu wa Disemba zilipoanza, kumeshuhudiwa uhaba mkubwa wa mboga za majani pamoja na nyanya jambo ambalo limewatatiza wakaazi wa eneo hilo.
"Nyanya kubwa moja kwa sasa ni shilingi 35 ikilinganishwa na hapo awali ambapo ilikuwa inauzwa shilingi 10," amesema mchuuzi huyo.
Ameongeza kusema kuwa baadhi ya wanunuzi kwa sasa wameamua kutumia nyanya ya mkebe ambayo inauzwa shilingi 20 na kuna ile ya pakiti inyouzwa shilingi 15.
Amesema kuwa wameamua hivyo baada ya kushindwa kununua nyanya kwa bei yake hiyo kali.
Hata hivyo mwenyekiti wa soko kuu ya Kongowea mjini Mombasa amesema kuwa hali hiyo itaendelea mpaka sherehe za mwaka mpya zitakapoisha kwa sababu baadhi ya magari ya kusafirisha bidhaa za soko hazihudumu kufuatia waendeshaji kujumuika na wenzao katika sherehe hizo za kila mwaka.
Mwenyekiti huyo wakati huo huo amewaomba wenyeji kuivumilia hali hiyo kwa muda mpaka pale shughuli za kawaida zitakaporejelewa.