Wakaazi wa eneo la Pwani wameshinikizwa kuungana pamoja na kujiandaa kwa uchaguzi wa mwaka wa 2017 katika mchakato wa kisiasa.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mwenyekiti wa Chama cha Federal Party of Kenya eneo la Pwani Omar Mohammed Kuta aliwasihi viongozi wa eneo la Pwani kuwa makini na kukomesha tabia yao ya kujiunga na vyama vilivyobuniwa katika maeneo mengine ya nchi.
Bw Kuta alisema chama hicho cha Kipwani kinastahili kuungwa mkono na Pwani wote na kushirikiana kwa karibu mno ili kuona kwamba mikakati mwafaka inaidhinishwa na kuingia uongozini kwa kutumia chama hicho cha Kipwani.
Aidha, Kuta alisema kwamba chama hicho tayari kiko thabiti na kinaendelea kusambaza mikakati yake mashinani katika juhudi za kuwarai Wapwani kujiunga na chama hicho na kuleta mwamko mpya kwa majamii ya wapwani mashinani.
“Tafadhalini viongozi wa kisiasa wa eneo la Pwani lazima muwe makini sana na kusitisha tabia ya kujiunga na vyama vilivyobuniwa na jamii zingine kwani hatua hiyo haita leta ule umoja wa wapwani," alisema Kuta.
Mwanasiasa huyo alishikilia kwamba chama hicho kamwe hakitarudi nyuma katika kuwaunganisha Wakaazi wa Pwani kisiasa bila kitahakisha kwamba uchaguzi ujao kimeta mabadiliko makubwa ya kidemokrasia.