Share news tips with us here at Hivisasa

Watu wanaosafiri wakati huu wa sherehe wametakiwa kuwa waangalifu kutokana na matapeli wanaojifanya wahudumu wa mabasi na kuwapora abiria pesa.

Hii ni baada ya idara ya trafiki eneo la Pwani kutangaza kuwa wamegundua kuna kampuni zinazojitokeza na kudai kuwa wana mabasi ya kusafirisha abiria na kisha kuwadhulumu pesa zao.

Katika taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, afisa wa wa trafiki wa kitengo cha dharura eneo la Pwani Solomon Njuguna aliwataka abiria kudhibitisha uhalai wa kampuni kabla kuabiri gari lolote.

“Uchunguzi wetu umebaini kuna watu wanajifanya wahudumu wa mabasi na wakipewa pesa wanatoroka, kitu tunaomba ni abiria kudai kuonyeshwa kadi maalum kudhibitisha kuwa ni mhudumu wa kweli,” alisema Njuguna.

Afisa huyo amewaomba wale wanaoshuku kampuni yoyote ya mabasi kuwa si halali waripoti kwa polisi ili uchunguzi ufanyike mara moja.

Pia vile vile amewataka madereva kuwa makini barabarani wakati huu wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya ambapo idadi kubwa ya watu wanasafiri maeneo mbalimbali.