Washukiwa wanne wanaotuhumiwa kwa kushirikiana na kundi la Al- shaabab walioshikwa katika barabara ya Bumala Kaunti ya Busia wakielekea nchini Uganda wamefikishwa mahakamani mjini Mombasa kwa kosa hilo.
Washukiwa hao Mohammed Abdalla, Faraj Fahim, Ali Omar na Kassim Ahmed ambao hawakuruhusiwa kujibu mashtaka wamewekwa korokoroni na hakimu mkaazi Diana Mochche hadi tarehe 7 mwezi ujao wakati kesi hiyo itakapotajwa.
Hakimu mkazi Mochache ametoa uamuzi huo baada ya kiongozi wa mashtaka kuomba mahakama iwapatie muda zaidi maafisa wa polisi ili kutimiza uchunguzi wao dhidi ya washukiwa hao.
Wakati uo huo washukiwa wanne wanaotuhumiwa kwa kosa la mauaji katika kijiji cha Nzombo wilayani Kinango kaunti ya Kwale wamefikishwa mahakamani mjini Mombasa na kukanusha kosa hilo.
Washukiwa hao Kwekwe Luganje, Mwaka Luganje, Machemunda Mboga Malembi na Masha Wanje Mwadori hawakupewa ruhusa ya kujitetea mbele ya Hakimu Asenath Ongeri mpaka tarehe 4 mwezi ujao kesi hiyo itakapotajwa huku wakisalia korokoroni.
Shtaka dhidi yao ni kuwa kati ya tarehe 28 na 29 mwezi wa Novemba mwaka jana katika kijiji cha Nzombo kaunti ya Kwale wilayani Kinango kinyume cha sheria wanne hao pamoja na wengine ambao hawako mbele ya mahakama walimuua Luganje Mwandori Luganje.