Share news tips with us here at Hivisasa

Imebainika kuwa hakuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa washukiwa wawili waliokamatwa kwa tuhuma za mauwaji ya Mpeketoni ya mwaka 2014, wana uhusiano na kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Kauli hii ilitolewa na Jeremia Ikiao, afisa mkuu wa upelelezi wa Kaunti ya Tana River siku ya Jumatano, alipokuwa akitoa ushahidi wake katika Mahakama kuu ya Mombasa.

Ikiao alisema kuwa washukiwa Mahadi Swaleh na Diana Salim, si tishio katika usalama wa Lamu na taifa kwa jumla.

Aliongeza kuwa hawakupata silaha zozote wala vilipuzi walipo chunguza makaazi ya wawili hao.

Aidha, alisisitiza kuwa Mahadi Swaleh si mliki wa magari mawili yaliyotumika katika kutekeleza ugaidi huo kama inavyodaiwa.

Wakati huo huo, afisa huyo alishindwa kutoa majina ya maafisa wa GSU anaodai walitumiwa na Mahadi Swaleh katika kuwanyanyasa wakaazi wa Maporomokoni kwenye mzozo wa ardhi baina ya mshukiwa na wakaazi wa shamba hilo.

Mahadi Swaleh na Diana Salim wanakabiliwa na kesi ya ugaidi na mauwaji ya watu 60 kwenye shambulizi liliotokea eneo la Mpeketoni mwaka 2014.