Wanaume wawili wanaokabiliwa na shtaka la mauaji wameachiliwa huru baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha katika Mahakama kuu ya Mombasa.
Washukiwa hao, Saidi Charo na Karisa Kambi, wanadaiwa kumuua kwa kumdunga kisu marehemu Kazungu Kuro Kambe huko Miwaleni, eneo la Kaloleni, kati ya Septemba 8 na 10 mwaka wa 2013.
Akitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi, jaji katika mahakama kuu ya Mombasa, Martin Muya, alisema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha dhidi ya washukiwa hao na kuamuru wao kuachiliwa huru kwa mujibu wa katiba.
Wawili hao walijawa na furaha huku wakitabasamu baada ya kusikia uamuzi huo.