Share news tips with us here at Hivisasa

Wasimamizi wakuu wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa TUM, wametakiwa kufika mbele ya Kamati teule ya elimu ya bunge la Kaunti ya Mombasa kujadili chanzo cha maandamano ya wanafunzi wa chuo hicho ili kupata suluhu la haraka.

Kwenye mkutano ambao ulifanyika siku ya Jumatatu katika ukumbi wa mijadala katika ofisi kuu za bunge hilo, baina ya wanachama kutoka bunge la Mombasa na viongozi wa wanafunzi wa chuo cha TUM, viongozi hao wa wanafunzi waliweka lawama kwenye mamlaka ya chuo hicho.

Viongozi hao walilaumu wakuu wa chuo hicho kwa kutowasikiliza na kufanya maamuzi ambayo yanapendelea upande mmoja bila kuzingatia athari kwa upande wa wanafunzi.

Mwakilishi wa Wadi ya Bofu, Suleiman Boma, ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, alisema kuwa wataweka tarehe ambayo wawakilishi kutoka mamlaka ya chuo watakutana na kamati hiyo baada kutuma mawasiliano rasmi kwenye chuo hicho.

“Nashukuru viongozi wa wanafunzi kwa kuonyesha subira, hata baada ya mkutano kati yetu na wao kuahirishwa zaidi ya mara tatu. Tumesikia upande wao na itakuwa zamu ya usimamizi wa chuo hicho cha TUM kualikwa na kuja mbele ya kamati ili tujadili njia mwafaka ya kupata suluhu kwenye suala hili,” alisema Boma.

Kwa upande wa viongozi wa wanafunzi wakiongozwa na mwenyekiti wao Desmond Ocharo walisema wako tayari kupata suluhu la haraka kwenye zogo hilo iwapo watahusishwa nachuo hicho kwenye uamuzi wao na kutatua suala lililosababisha mgomo huo.