Licha ya baadhi ya nchi za ulaya kuwaonya raia wao dhidi ya kutembelea nchi za Afrika Mashariki, eneo la Pwani limethibitisha kuendelea kupokea idadi kubwa ya watalii katika msimu huu wa likizo ya Desemba na mikahawa yote imeorodhesha idadi nyingi ya watalii.
Akiongea kwenye ofisi yake siku ya Jumatatu jijini Mombasa, mkurugenzi wa muungano huo wa watalii Mohammed Hersi alisema kuwa wanatarajia kuendelea kupokea wageni kutoka kila nchi na hata watalii kutoka nchini wanaalikwa kufanya utalii katika nchi yao.
Mkurugenzi huyo alizitaka nchi zote za ulaya na Marekani kufutilia mbali hofu na kuwaomba kuwa huru kutembelea nchi ya Kenya, na usalama katika eneo la Pwani uko imara kinyume na nyakati za awali.
Alichukua nafasi hiyo na kuwashukuru watalii ambao wanaendelea kuchukua nafasi zao katika hoteli za kitalii katika miji ya Pwani ambayo inapokea watalii.
Alionyesha furaha yake kwa kuona kuwa baadhi ya nchi zina imani na nchi hii na kudokeza kuwa jinsi hoteli pamoja na mikahawa inaendelea kujaa wageni, huenda kukaingia wageni wengi hata nafasi zipungue.
Maeneo mengi katika eneo la Pwani kama vile Malindi, Mombasa, pamoja na miji ya eneo la South Coast huwa maarufu kwa kupokea watalii wengi kila mwisho wa mwaka, na hufaidi sana wenyeji ambao hujihusisha na kuwauzia bidhaa mbali mbali za kiafrika.