Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa wa uvuvi katika kaunti ndogo ya Naivasha Mathew Ngila amewaonya baadhi ya watalii wanaozuru ziwa Naivasha dhidi ya kujihusisha na shuguli za uvuvi haramu ziwani humo.

Ngila alisema kuwa baadahi ya wataali haswa wa asili ya Kichina wanashiriki shuguli za uvuvi ziwani humo kinyume cha sheria.

Akiongea afisini mwake siku ya Alhamisi, Ngila alisema kuwa baadhi ya wavuvi wenyeji wanawasaidia watalii hao kutekeleza uhalifu huo kwa kisingizio cha kutaliii ziwa hilo.

Alisema kuwa wamegundua baadhi ya wavuvi hukodisha boti zao kwa watalii wa Kichina ambao baadaye huingia ziwani na kuvua samaki.

“Kuna watu wanakuja hapa kama watalii lakini wanapoingia ziwani, wanageuka kuwa wavuvi wa samaki na wanasaidiwa kutekeleza hilo na wavuvi wetu hapa baada ya kuwahonga kwa pesa kidogo,” alisema Ngila.

Aliongeza, “Tunawaonya wavuvi ambao watapatikana wakishirikiana na wageni hao kwamba wote watachukuliwa hatua za kisheria pamoja na vyeti vyao vya uvuvi kufutiliwa mbali.”

Aliwataka wenyeji wa eneo hilo kuwa macho na kuwaripoti watalii watakao onekena wakiendesha shuguli za kuvua samaki ziwani Naivasha.

“Ni jukumu la watu wanaokaa karibu na ziwa kuwa walinzi wa raslimali hii na kuripoti mtu yeyote ambaye kwa njia moja ama nyingine anakiuka sheria za kuendesha shuguli katika ziwa hili la Naivasha,” alisema Ngila.