Vijana wawili walifikishwa mbele ya mahakama moja ya Nakuru kujibu shtaka la wizi wa mabavu.
Washukiwa hao, Gordon Omondi na mvulana mwenye umri wa miaka 14, walishtakiwa na wengine Antony Nganga, Nahashon Ngare na mvulana mwingine mwenye umri wa miaka 15 kwa madai ya kutumia nguvu kumnyanganya Jeff Mwangi baisikeli yake yenye dhamani ya Sh12, 000 mnamo Januari 3, 2016 mjini Nakuru.
Aidha, walikabiliwa na mashtaka mengine ya kuiba simu mbili aina ya Neon na Nokia lumia, zote zenye thamani ya shilingi 16,300 kutoka kwa Mary Ngendo na Lillian Mugo, mnamo Januari 6, 2016 katika mtaa wa Freehold viungani mwa mji wa Nakuru.
Watano hao walikanusha madai hayo siku ya Ijumaa mbele ya Hakimu Mkaazi Judicaster Nthuku.
Hata hivyo Gordon Omondi, Antony Nganga na Nahashon Ngare waliachiliwa kwa bondi ya shilingi laki moja au pesa taslimu za kiwango sawia.
Watatu hao watazuiliwa katika rumande ya gereza la Nakuru GK Prison ikiwa watashindwa kulipa pesa hizo.
Upande wa mashtaka ulitaka mahakama kuzuia wavulana wawili waliokua chini ya miaka 18 katika rumande ya watoto.
Kesi hiyo itasikilizwa tarehe Machi 1, 2016.