Wakazi wa Kaunti ya Nyamira wanaochukua mikopo kutoka kwa benki ya Equity wamehimizwa kuhakikisha wanerejesha mikopo hiyo ili kusaidia benki hiyo kuwahudumia vyema.
Akihutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumatatu, meneja wa mauzo wa benki hiyo tawi la Keroka Robert Abere alisema kuwa mazoea ya watu kuchukua mikopo na kutoirejesha kwa wakati unaofaa ni hali ambayo inalemaza utoaji huduma kwa wakenya wateja wengine.
“Hii tabia ya watu kuchukua mikopo kutoka kwa benki na kisha kutoirejesha kwa wakati kwa hakika ni hali ambayo imekuwa ikilemaza utoaji huduma kwa wateja wengine,” alisema Abere.
Abere aliongeza kwa kuwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuhakikisha kuwa wanarejesha mikopo kwa wakati unaostahili, huku akiwahimiza wengine kujitokeza kuchukua mikopo ili kuendelesha biashara zao.
“Itakuwa vyema iwapo wateja wetu watarejesha mikopo kwa wakati unaofaa ili kwamba tuwahudumie wengine, na himizo langu kwa wateja wengine hasa makundi ya kibiashara kujitokeza kuchukua mikopo ili kuendelesha biashara zao,” aliongezea Abere.