Watoto walio kwenye makao ya Nakuru Childrens Remand Home iliyo Bondeni viungani mwa mji wa Nakuru wamepata sababu ya kutabasamu baada ya kupata krismasi ya mapema kutoka kwa wanachama wa muungano ya kikatoliki.
Toleo hilo lilitoka kwa makundi ya Catholic Women Association (CWA) na muungano wa kikatoliki na wanaumme wa Catholic Men Association (CMA).
Mratibu wa walei (Lay Apostolate Coordinator) katika jimbo katoliki la Nakuru Ronald Sunguti aliyeongoza miungano hiyo kwenye shughuli hiyo alisema lengo lao la kuwatembelea watoto hao lilikuwa kuwafanya wajihisi kwamba kuna watu wanaowajali na kuwapenda.
"Sababu ya kuja hapa ni kwamba tulitaka kuwaletea watoto hawa krismamsi ya mapema na tuwajuze pia kuwa wanapendwa na wazazi wao pamoja na kwamba wanapendwa na kanisa katoliki. Pia, tumekuja kuwatangazia watoto hawa kuzaliwa kwa mwokozi Yesu Kristu kwamba ingawa wako hapa, Yesu Kristu pia ataweza kuzaliwa moyoni mwao," alisema Sunguti.
Sunguti hata hivyo ametoa wito kwa wote kuonyesha ukarimu wao kwa kuwatembelea wote kutoka familia maskini na pia watoto wanahitaji msaada haswaa wakati huu wa krismamsi.
"Wito wangu ni kwa wote kuwashirikisha na pia kuwakumbuka wale ambao hawajafanikiwa pakubwa kwenye Jamii . Pia wakenya wanafaa kuwakumbuka wale wanaohisi kama wametengwa kwenye Jamii," aliashiria Sunguti.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo iliyofanywa Alhamisi, meneja wa rumande hiyo ya watoto Lorna Sang alisimulia kufurahishwa kwake na kitendo hicho ambacho alikitaja kama cha kikarimu.
"Tumetembelewa na akina mama na wanaumme kutoka kanisa katoliki ambao nilizungumza nao kupitia kwa mratibu wa kitengo cha walei Sunguti na kutokana na hilo, waliweza kujiandaa na wakaja kututembelea. Watoto wamefurahia sana kwa kuwa wameweza kutuandalia chakula cha mchana na pia wameweza kutuletea vitu mbalimbali kama vile sabuni na mafuta. Tunawashukuru sana na Mungu awabariki," alidokeza Sang.
Watoto walio kwenye rumande hiyo kwa upande wao nao hawakuweza kuficha furaha yao, huku wakiwaombea wote waliowatembelea baraka zake Mola.