Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Bi Mishi Mboko amesema kwamba kwa kiwango kikubwa watoto wanaoranda randa mtaani ndio wanaolengwa zaidi na makundi ya kigaidi ili kujiunga na kuhatarisha usalama wa nchi.

Mboko amesema kwamba ongezeko hilo la watoto wa kurandaranda mitaani na ambao hawana namna ya kupata mahitaji maalum ndio wamo katika hatari ya kujipata katika makundi ya kigaidi, na akawataka maafisa wa polisi kuchunguza hali hiyo na kuidhibiti.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumma, kiongozi huyo alihoji kwamba watoto wa kurandaranda mitaani mjini Mombasa kwa sasa wamekuwa wakubwa, na njia yao rahisi ya kujipatia mahitaji ya kimsingi ni kupitia kwa uhalifu, hali ambayo imechangia wengi wao kujiunga na maswala ya kigaidi.

Ameitaka Serikali kuu kushirikiana na ile ya kaunti ya Mombasa ili kuhakikisha kwamba swala hilo linakabiliwa na kuimarisha usalama wa kaunti hiyo.

"Tunaiomba serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa kushirikiana kwa karibu mno na kuwatafutia makao watoto hawa ili kuzuia kukithiri kwa visa vya kihalifu na ugaidi vinachangiwa na watoto hao kujiunga na makundi ya kigaidi," alisema Mboko.

Kauli ya kiongozi huyo inajiri baada ya afisa wa maswala ya kijinsia na haki za watoto katika Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini  MIHURI Topista Juma kusema kwamba watoto hao wamo katika hatari ya kusajiliwa katika makundi ya kigaidi.