Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Watoto wanaorandaranda mitaani mjini Mombasa wanataka serikali kuwapa ulinzi kwani wanadai kuwa wanateswa na kuhangaishwa na maafisa wa polisi. 

Watoto hao ambao wengi wao huishi katika eneo la Backstan mjini Mombasa, wanasema maafisa hao huwachapa nyakati za usiku huku wakidai kuwa wao ni wezi.

"Sisi sio wezi, tunakula tu vyakula vilivyotupwa. Wakati mwingine tukibahatika tunapewa na wasamaria wema,'' alisema mmoja wao.

 Watoto hao sasa wanaomba serikali, wahisani na viongozi wa kanisa kuwapa ufadhili ili waweze kujikimu kimaisha bila kuvitegemea vyakula wanavyookota kwenye mapipa.

Ni hivi majuzi tu ambapo kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kuwa watoto wanaorandaranda mtaani wapo katika hatari ya kusajiliwa kujiunga na makundi ya uhalifu na ugaidi likiwemo kundi la Al Shabaab.