Share news tips with us here at Hivisasa

Watoto wawili waliopatikana jijini Kisumu baada ya kudaiwa kuachwa na baba yao, walifikishwa katika mahakama ya Winam jijini Kisumu siku ya Jumatano kutoa ushahidi wao.

Wakitoa ushahidi wao mbele ya Hakimu Johnston Mitey, watoto hao walisema kuwa walifunga safari na baba yao kutoka eneo ambalo hawakulitaja mnamo Desemba 27, 2015, kuelekea eneo la Kanyabundi, mjini Kendubay, Kaunti ya Homabay.

Walisema kuwa walipofika katika kituo kikuu cha magari jijini Kisumu, walishuka kwenye gari walimokuwa wakisafiria, ambapo baba yao aliwaambia kuwa alikuwa anaenda msalani na kuwaacha katika kituo hicho.

Watoto hao wenye umri wa kati ya miaka saba na miaka kumi, walisema kuwa walimsubiri baba yao lakini hakurejea.

Watoto hao waliokolewa na msamaria mwema aliyewapeleka katika Kituo kikuu cha polisi jijini Kisumu.

Watoto hao wanaendelea kuishi kwenye Makao ya watoto ya Mama Ngina jijini Kisumu, huku juhudi za kumsaka baba yao zikiimarishwa na maafisa wa polisi.