Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Watoto wawili walitekwa nyara na watu wasiojulikana katika eneo la Ruiru walipokuwa wakielekea shuleni siku ya Ijumaa.

Watoto hao kutoka Shule ya msingi ya Ruiru Township walitekwa nyara mita kadhaa kutoka kwa lango la shule hilo.

Walioshuhudia kisa hicho walidai kwamba wawili hao waliingizwa katika gari aina ya probox na mwamamume mmoja akishirikiana na mwanadada na walikuwa wamejifunika nyuso zao.

Akidhibitisha tukio hilo, afisa mkuu katika eneo la Ruiru Isaac Thuranira alisema kuwa polisi wameanzisha uchunguzi dhidi ya tukio hilo.

Alisema kuwa utekaji nyara miongoni mwa watoto wa shule za msingi umeongezeka.

Thuranira alisema kuwa waliweza kupata nambari ya usajili ya gari hilo kutoka kwa raia mmoja aliyeshuhudia kisa hicho.

Hata hivyo, alisema kuwa wazazi wanafaa kuwapeleka watoto shuleni ili kuzuia matukio ya aina hiyo.

Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa watekaji nyara mara nyingi huwaitisha wazazi wa watoto pesa na kuwakanya wazazi dhidi ya kufuata maagizo ya majambazi hao.

Thuranira alisema kuwa wazazi wa watoto waliotekwa nyara wanapaswa kuwasilisha ripoti wanapopokea simu ama mawasiliano yoyote kuhusu watoto hao.

"Nataka kuhakikishia wakazi kuwa idara ya polisi itapambana na uhalifu wa aina hii katika eneo hili vilivyo. Nawaomba pia muwe wenye mawasiliano na polisi ili kutusaidia kupambana na uhalifu," alisema Thuranira.

Alisema kuwa wakuu wa shule na wazazi wanafaa kuweka mikakati ambayo itahakikishia watoto usalama wao.