Kamishna wa kaunti ya Nyamira Josphine Onunga na mwenzake wa kaunti ya Bomet Benard Leparmaria wamejitokeza kuwaomba wakazi wanaoishi kwenye mpaka wa Nyamira na Bomet kuwa watulivu uchunguzi unapoanzishwa kubaini chanzo cha baadhi ya nyumba za jamii ya Abagusii na Kipsigis kuteketezwa Alhamisi wiki jana.
Wakihutubu katika eneo la Riontonyi siku ya Jumapili, makamishna hao waliwaomba wakazi wa eneo hilo la Borabu kuwa watulivu na kukumbatia mazungumzo ya amani ambayo tayari yameanzishwa na serikali za kaunti hizo mbili.
"Isije ikawa kwamba kila mara tukiwa na tofauti miongoni mwetu suluhu ni kushiriki kwenye vita ikizingatiwa kwamba tunaweza suluhisha tofauti zetu kwa kufanya mazungumzo ya amani kwa maana vita havileti maendeleo na ndio maana sharti tuishi pamoja kwa amani," alisema Onunga.
Kwa upande wake kamishna wa kaunti ya Bomet Benard Leparmaria, ni mhimu wananchi kukumbatia amani na maridhiano, huku akisisitiza kuwa kamwe serikali haitovumilia vita baina ya jamii hizo mbili.
"Kukumbatia amani na maridhiano ni kigezo muhimu sana na kamwe vita havitotusaidia kwa lolote na hakika la muhimu ni kwa kwetu sisi kuishi kwa amani na kwa maana serikali imepiga hatua kubwa kuwahimiza wananchi kuzingatia amani kamwe hatutoketi nakuona wananchi wakipigana," aliongezea Leparmaria.
Haya yanajiri baada ya watu watono kujeruhiwa kwenye makabiliano baina ya jamii hizo mbili Alhamisi wiki jana, jamii ambazo kwa muda sasa zimekuwa zikishtumiana kwa wizi wa mifugo kwenye eneo hilo.