Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Watu wanaoishi na ulemavu kaunti ya Nakuru wanaitaka serikali kuu kuharakisha utekelezaji wa sheria ambayo bado inasubiri kupitishwa bungeni, ili walemavu waweze kupata huduma muhimu katika majengo ya umma sawia na wananchi wengine.

Wengi wao wanadai kunyanyasika kimaisha, kwani kulingana na muundo wa majumba mengi ya umma mfano yale ya benki, shule na hata hopitali, hayana milango inayoweza kuwaruhusu kuingia ndani kwa urahisi kutafuta huduma muhimu.

Akizungumza na mwandishi huyu Jumatano afisini mwake, Mwenyekiti wa muungano wa watu wanaoishi na ulemavu (APDK ) Bw Fred Owako, amesema kuwa bunge la kitaifa linafaa kuangazia sheria hiyo kwa udharura kwani watu wanaoishi na ulemavu bado wanapitia changamoto wakati wanatafuta huduma katika afisi mbalimbali kwenye kaunti kutokana na baadhi ya majengo kuwa na maghorofa mengi na kuwa vigumu kwao kupata huduma wanazohitaji.

“Tunaomba bunge liweze kutekeleza sheria hiyo kwa haraka kwa sababu, kama walemavu, tunapitia changamoto katika baadhi ya majengo wakati wa kutafuta huduma,” Owako alisema.

Itakumbukwa kuwa mwaka uliopita mwenyekiti huyo aliwaandikia wamiliki wa majengo ya umma na yale ya kibinafsi, akiwataka kuweka kambarau(lifti).

Vile vile ameiomba wizara ya mipango maalum nchini kushinikiza bunge la kitaifa kuharakisha utekelezwaji wa sheria hiyo.