Idadi kubwa ya watu wanaohama kutoka vijijini ndio chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa makazi duni katika mitaa mbali mbali kwenye Kaunti ya Mombasa.
Akihutubu katika hafla ya uzinduzi ramsi wa utaratibu na mpangilio wa kuboresha jiji la Mombasa siku ya Jumatano, waziri wa ardhi katika Kaunti ya Mombasa Francis Thoya alisema kuwa kwa wakati wa karibuni, watu kutoka sehemu tofauti wamekuwa wakimiminika kwa wingi kwenye jiji hilo, ambapo wengi wao huwa wanawasili kuja kutafuta kazi.
Thoya alisema kuwa hali hiyo huwafanya wengine kuhiari kuishi kwenye nyumba za mabanda na zisizo za kudumu, ambazo huwa nafuu kulipia kodi.
Waziri huyo alisema kuwa serikali ya Kaunti kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa kama JICA, ambalo linatoka nchi ya Japan, watahakikisha kuwa maeneo ya vitongoji mbalimbali kwenye kaunti hiyo kuna makazi bora na yenye viwango vya mataifa.
Kwenye mkutano huo, ambapo pia uliwakilishwa na maafisa kuto Benki ya Dunia, Kaunti ya Mombasa inalenga kuweka mikakati ya kuliona jiji la Mombasa likiimarika katika muda wa miaka arobaini katika sekta za uzoaji taka, mipangilio ya majengo pamaoja na miundomsingi kwa jumla ili kupunguza hali ya misongamano na kuliweka jiji hilo la kitalii kuwa safi kama zamani.
Aidha, Naibu wa Gavana wa Kaunti hiyo Bi Hezel Katana alisema kuwa watajitahidi kulikomaza jiji hilo na kufuata nyayo za miji ambayo imeendelea kutoka nchi nyingine duniani.