Share news tips with us here at Hivisasa

Wavuvi ambao hufanya shughuli yao ya kuvua samaki katika bahari Hindi wametoa wito kwa serkali ya Kaunti ya Mombasa kununua samaki na kuwasaidia kutafuta soko la moja kwa moja badala ya kuendelea kuuza samaki kwenye masoko ya karibu na kwa bei ya rejareja hali ambayo haiwatoshelezi katika mfumo wa kufaidi kiuchumi.

Walisema kuwa mara nyingi wao ndio hujitafutia soko la bidhaa zao na huwa vigumu wakati mwingine kwa sababu ya wengi wa wateja wao lengwa kuwa na mtazamo finyu kuhusiana na bei ya kununua samaki ambako wengi hukejeli bei kwa sababu wengi wa wateja wao ni wa mapato ya chini na hawana uwezo wa kununua samaki kwenye bei ya juu.

Wakiongozwa kwenye mahojiano katika fukwe za Shelly huko Mombasa siku ya Jumapili, mwenyekiti wa kikundi cha wavuvi hao, Juma Lewa, alisema kuwa hawana soko kubwa la kuuza samaki wao mbali na kuuzia wenyeji hasa wale wanaochoma na kuranga samaki katika masoko ya mitaa ya Likoni, Mtongwe, na soko kuu la Kongowea na si wote hukubaliana na bei yao.

Juma alisema itakuwa nafuu kwao iwapo idara ya samaki na uvuvi kwa ushirikiano na wizara ya biashara na ile vijana kwenye Kaunti ya Mombasa ingeingilia kati kwa kununua samaki na kutafuta soko la kuuza samaki wao ambao ndio tegeo kuu na kitega uchumi kwa vijana hao.

Walimtaka gavana wa Kaunti ya Mombasa Bwana Ali Hassan Joho kutimiza ahadi yake vile aliwahidi vijana kuwa atahakikisha kila makundi ya vijana wanatafutiwa masoko ya kuuza bidhaa zao ili kujikimu maishani.

“Tunamwomba gavana wetu kuchukua hatua na kushirikiana na wizara husika na kutufaidi jinsi alivyoahidi nyakati za kufanya kampeni za kuwania kiti cha ugavana,” alisema Juma.