Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wawakilishi wa maeneo wadi mbalimbali nchini wameshtumiwa kwa hali ya kukithiri kwa ufisadi kwenye serikali za kaunti nyingi nchini. 

Akihutubia kina mama huko Borabu, kaunti ya Nyamira siku ya Jumatatu, seneta mteule Daisy Nyongesa alisema kuwa bunge la seneti hutegemea sana ripoti za mhasibu wa pesa za umma ili kuchunguza madai ya ufisadi kwenye serikali za kaunti mbalimbali, ilhali kuna wawakilishi wa wadi wanaofaa kuchunguza matumizi ya fedha kwenye serikali husika.

Aliongeza kusema kuwa kuna shtuma nyingi za ufisadi ambazo hazijakuwa zikiwasilishwa bungeni, na akashangazwa na kujitolea kwa wawakilishi wadi kupambana na ufisadi. 

"Ni aibu kuwa tunazungumzia ufisadi serikalini ilhali kuna wawakilishi wadi wanaofaa kuwachungiza maafisa mbalimbali wa serikali za kaunti, na kwa kweli bunge la seneti limekuwa likipata ripoti za ufisadi kwenye serikali za kaunti kupitia kwa vyombo vya habari na afisi ya mhasibu wa pesa za umma, hali inayoibua maswali ikiwa kweli wawakilishi wa wadi wanatekeleza majukumu yao inavyofaa," alishangazwa Nyongesa. 

Seneta huyo aidha alisema kuwa wakenya wengi wamepoteza imani na serikali za kaunti kufuatia ufisadi unaoendelea kukithiri kwenye idara mbalimbali za serikali za kaunti, ila akawaomba wawakilishi wa wadi kutotumia mamlaka yao kuwakandamiza magavana. 

"Hatukugatua ufisadi, na wanachohitaji wakenya ni kutekelezwa miradi mbalimbali mashinani. Lakini ili ufisadi kukabiliwa sharti wawakilishi wadi wajitolee kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kutowakandamiza magavana," alimalizia kusemaa.