Mwakilishi mteule katika kaunti ya Nakuru Ruth Cheptarus sasa ametaka vazi la hijab kutohusishwa na swala la utekelezaji wa mashambulizi, huku akisema kwamba vazi hilo lina lengo la kustiri wanawake wa kiislamu.
Anasema kwamba baadhi ya wakenya wamekuwa wakiwachukuliwa wanawake wa kiislamu wanaovaa vazi hilo kama wahalifu, huku wengine wakiwagandamiza kutokana na uuvaji wake.
Ingawa amekiri kwamba baadhi ya wahalifu wamekuwa wakinunua vazi hilo ili kulitumia kutekeleza maovu yao, sio wote wanaovaa vazi hilo ambao ni wahalifu.
Ameongeza kwamba kanzu zinazovaliwa na waislamu pamoja na kofia zao huuzwa pia madukani na zinaweza kununuliwa na yeyote yule kwani hakuna hitaji la kujua iwapo anayenunua mavazi hao ni muumini wa dini ya kiislamu, jambo ambalo wahalifu hulitumia kutekeleza maovu hao.
Hata hivyo, ametaka mavazi hayo kutonunuliwa kwa lengo hilo la utekelezaji wa uhalifu.
Kulingana naye, mavazi hayo ya kiislamu yamewapelekea wengi kuwashuku kuwa wahalifu, miongoni mwao wakiwa maafisa wa polisi anaosema kutumia muda wao mwingi kuwapekua katika maeneo yanayofanyiwa upekuzi.
Ni matamshi ambayo yameungwa mkono na mwakilishi mwingine mteule klatika kaunti ya Nakuru kwa jina la Hawa Ibrahim Hassan, huku akisema mhalifu hana dini wala kabila.
Walisema hayo walipokuwa wakizungumza na mwandishi huyu kwenye mahojiano ya kipekee Alhamisi hii mjini Nakuru.