Wawakilishi wadi kutoka Nyamira wameunga mkono muungano wa Cord unaongozwa na Raila Odinga kwa kukemea ufisadi serikalini.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, wawakilishi wadi hao wakiongozwa na Peter Maroro, walimuunga mkono Raila Odinga kwa kukemea ufisadi serikalini na kuzua maswali kuhusu jinsi pesa za Eurobond zilivyotumika.
Wawakilishi hao walisema kuwa bila upinzani, serikali haiwezi simama imara na kuwajibikia utumizi wa pesa za umma.
Waliitaka serikali kueleza jinsi pesa za Eurobond zilitumika kufanya maendeleo nchini.
Aidha, wawakilishi hao walikosoa tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC, kwa kumtishia Raila Odinga na kumwagiza kufika mbele yao.
Walisema kuwa kile EACC inastahili kufanya ni kufuatilia yale Raila aliyosema ilikuweza kubaini ukweli kuhusu tetesi hizo.
“Si vizuri tume ya EACC kumwagiza kiongozi wa upinzani Raila Odinga kufika mbele yake kueleza ushahidi wake kuhusu jinsi pesa za Eurobond zilitumika,” alisema Maroro.
Wakati huo huo, wawakilshi hao walisema sharti serikali iwape viongozi wa upinzani uhuru wa kuikosoa serikali kama njia moja ya kulainisha mambo yanapoenda kombo.