Watu wawili wamekamatwa na maafisa wa kaunti na wale wa utawala kufuatia uuzaji haramu wa mbolea katika maduka ya Eldoret.
Akidhibitisha kisa hicho, afisa wa usalama katika kaunti, Bwana Paul Ruto, alisema kwamba walifahamishwa na raia wa eneo hilo kuhusu lori lililokuwa likisafirisha mbolea kwenye duka hilo.
“Niliona gari likibeba magunia kumi na pikipiki ikibeba magunia tatu ya mbolea kutoka duka hilo. Bado tunatafuta lori hilo ambalo lilileta mbolea kwenye duka hilo,” alisema Ruto.
Aliongeza, “Tulipata magunia 25 yamejaa mbolea, 10 yakiwa nusu na magunia 41 yalikuwa bure. Tunashuku biashara hii imekuwa ikiendelea kwa siku kadhaa.”
Ruto alisema kwamba wafanyibiashara hao wamekuwa wakipanga njama na wasimamizi wakuu wa bodi ya nafaka na chifu kuuza mbolea hiyo kwa bei ya juu.
Mwenye duka hilo alitoweka lakini maafisa wa polisi wameanza msako.
Bwana Kipkorir Menjo, mkurugenzi wa Chama cha wakulima nchini KFA, aliwahimiza wakulima kujihusisha na mashirika ya wakulima kuwawezesha kupata mbolea moja kwa moja ili kuzuia vitendo kama hivyo.
Menjo aliiomba serikali kupeleka magunia milioni moja ya mbolea kwa kaunti nne za bonde la ufa ili kuzuia ukosefu wa mbolea.
“Ukosefu wa mbolea ni tishio kubwa kwa uzalishaji wa chakula na mapato ya wakulima. Serikali haipaswi kuagiza chakula kutoka nchi za nje ilhali tunaweza kuza chakula chetu humu nchini,” alisema Menjo.