Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi katika Kaunti za Nyamira na Kisii wamepongezwa kwa kuitikia wito wa kutowakeketa watoto wasichana kwani ni kinyume na sheria.

Akizungumza mnamo siku ya Jumanne mjini Nyamira, mwenyekiti wa chama cha kupambana na ukeketaji kwa watoto wasichana nchini Linah Jebii Kilimo aliwapongeza wazazi wa kaunti hizo kwa kupunguza visa vya kuwakeketa watoto wasichana katika jamii ya Kisii.

Kulingana na Kilimo, hakuna haja ya watoto wasichana kutahirishwa, jambo ambalo limeonekana kupokelewa kwa njia iliyo na manufaa katika sehemu mbalimbali za Kisii, na kuomba mila za kale zitupiliwe mbali na kusahaulika.

“Zamani mkisii alikuwa anatahirisha mtoto msichana kwa lazima, lakini tangu tuanze kukemea na kukataa ukeketaji kwa watoto wasichana kumeonekana mabadiliko makubwa hapa Kisii,” alisema kilimo.

“Napongeza wazazi kwa kuitikia wito wetu wa kukana watoto wasichana kutotahirishwa kwani ni kinyume na sheria na ninaomba muendelee hivyo hivyo,” aliongeza Kilimo.

Hata hivyo, Kilimo aliwashauri madaktari kutojihusisha na ukeketaji kwa watoto wasichana kwani ni kinyume na sheria na kusema daktari yeyote atafumaniwa akifanya kosa hilo atanyanganywa cheti cha udaktari kwani tayari amevunja sheria kwa kumtahirisha mtoto msichana.

“Mtoto msichana astahili kukeketwa kwani ni kumuharibu mtoto huyo, na kuna haja kwa watu kuacha mtoto msichana kuwa hivyo na madaktari nawaomba mlinde kazi yenu msijihusishe na ukeketaji huo,” alisisitiza Kilimo.