Zoezi la kuwapa watoto walio chini ya miaka mitano chanjo ya polio limekamilika katika Kaunti ya Nyamira huku wazazi wakipongezwa kwa kuwashirikisha wanao katika zoezi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa mjini Nyamira, mmoja wa wahudumu wa afya katika kaunti hiyo, Maryrose Moraa, alisema zozi hilo lililong’oa nanga siku ya Jumamosi limekamilika vyema bila kukumbwa na changamoto yoyote.
Mhuhudu huyo aliwapongeza wazazi kwa kushiriki katika zoezi hilo, ambalo alisema liliwanufaisha idadi kubwa ya watoto.
“Tulikuwa na zoezi la kuwapa watoto walio chini ya miaka mitano chanjo ya polio na limekamilika vizuri. Idadi kubwa ya watoto iliweza kupokea chanjo hiyo ambayo ni ya kipee kwa afya yao,” alisema Moraa.
Aliongeza, “Napongeza wazazi kwa kushirikiana nasi kuhakikisha watoto wao wamepata chanjo hiyo ambayo ni muhimu kwa watoto wachanga. Nawaomba waendelee kuwa na moyo kama huo na kuwaruhusu wanao kupokea chanjo hiyo.”
Aidha, mhudumu huyo alisema chanjo hiyo husaidia watoto kutolemaa kwani mtoto anapokosa chanjo hiyo ya polio, hukosa mengi na kwa bahati mbaya wengine huathirika na kuwa walemavu.
Wakati huo huo, mhudumu huyo alipongeza viongozi wa kanisa kwa kutozua isia mbalimbali dhidi ya chanjo hiyo jinsi ilivyoshuhudiwa hapo awali.