Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi ambao watoto wao huishi na ulemavu katika eneo la Rongai, wamelaumiwa kwa kuwaficha nyumbani watoto hao jambo ambalo linawafanya kutotambuliwa hata na serikali.

Akizungumza na mwandishi huyu Ijumaa, afisa mkuu wa leba na ustawi wa jamii eneo la Rongai Gitonga Mutiga amesema kuwa, wazazi hao wamewanyima watoto hao haki zao haswa ya kupata elimu.

“Kila mtoto humu nchini ana haki ya kupata elimu awe mlemavu ama buheri wa afya, ni haki yake kupata elimu na ni jambo la kutamausha kuona baadhi ya wazazi wakiwaweka watoto wenye ulemavu nyumbani,” alisema Bw Mutiga.

Aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, jamii nyingi katika maeneo ya Rongai kuwa na dhana kwamba kupata mtoto mwenye ulemavu ni laana, jambo ambalo sio la kweli.

Ametoa wito kwa wananchi pamoja na utawala wa mkoa kufahamisha afisi yake kuhusu watoto hao ili wapate msaada kutoka kwa serikali ya kaunti na serikali kuu.