Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Shirika la Elimu Yetu Coalition (EYC) limeweka wazi nambari ya simu isiyokuwa na malipo ili kutumiwa katika kuripoti visa vya walimu wakuu wanaotoza karo ya juu.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne, afisa katika shirika hilo linalopigania haki ya elimu ya wanafunzi hapa nchini, Catherine Asego alisema kuwa nambari ya 0800720940 itasaidia kuleta nidhamu katika shule za upili za umma ambazo zinatoza karo ya juu.

Asego alisema kuchukuliwa kwa hatua hiyo ni kutokana na kupitishwa kwa sheria ya elimu ya msingi ya mwaka wa 2013 inayotoa mwongozo wa karo za shule kwa shule za upili za umma.

“Iwapo mwalimu mkuu yeyote ataongeza karo kwa kiwango fulani, sharti apate idhini kutoka kwa wakuu wa elimu wakidhibitisha nyongeza hiyo,” alisema Asego.

Afisa huyo aidha amewataka wazazi kuwa maakini na kupiga chapa ya karo hizo ambazo ni za juu na kisha kuwasiliana na afisi hizo kwa hatua zaidi.

Asego aliwatahadharisha walimu wakuu ambao watatumia fursa hiyo kuongeza karo ili kujifaidi wenyewe, kwa kusema kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria.