Baraza la wazee la Gilgil Jumatano liliweka wazi malalamishi yao dhidi ya unyakuzi wa ardhi yenye ekari ishirini ambayo imetengewa kutengenezwa kituo cha utamaduni wa jamii ya Agikuyu eneo hilo.
Wazee hao kutoka Kiama Kiama wamesema kuwa ardhi hiyo inayopakana na shule moja ya kibinafsi ilitolewa na aliyekuwa Waziri hayati Njenga Karume, na ilifaa kutumiwa kwa ujenzi wa makao hayo ya jamii ya wakikuyu.
Mwenyekiti wa baraza hilo Harrison Waweru amesema kuwa waziri huyo alitwaa ardhi hiyo kutoka kwa shamba la Gema na walikuwa wakipania kujenga makavazi hayo ili iwasaidie vijana wa jamii hiyo.
Waweru amesema kuwa walikuwa na vyeti vya umiliki na kusema kuwa mmiliki wa shule hiyo alikuwa amekosa hata kutoa vyeti alivyo navyo.
“Jina la shamba hili ni Cultural Centre na kila sehemu imetengewa sehemu yake, yule anataka kunyakua anafikiria nini? Tunaomba serikali iingilie na kumwondoa mfanyibiashara huyo,” alisema Waweru.
Wazee wengine Sospeter Wamae na James Mbugua wamesema kuwa katu hawangekubali ardhi hiyo kuchukuliwa kwani wameilinda kwa miaka mingi na inafaa kuwanufaisha watu wengi.
Juhudi za mwandishi huyu kujaribu kuwasiliana na mmiliki wa shule hiyo hazikufua dafu kwani licha ya kumpigia simu mara kadhaa hakujibu.
Picha: Kulingana na kundi hilo la wazee, ardhi hiyo ilitengewa kituo cha utamaduni wa jamii ya Agikuyu eneo hilo kabla ya kunyakuliwa. Twitter.com