Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wazee wa Kaya katika eneo la Pwani wamekashifu hatua ya polisi ya kuwakamata vijana kwa madai kwamba ni wanachama wa kundi la MRC.

Wazee hao wanaowakilisha jamii ya wamijikenda inayopatikana katika ukanda wa Pwani ya Kenya walisema kuwa vijana wanaokamatwa sio wahalifu kwani wao hukamatwa bila ushahidi.

Wakiongea siku ya Jumanne, washirikishi wa kundi hilo la wazee walisema kwamba kuna vijana wanaojihusisha na uhalifu, lakini wakawataka polisi kufanya uchunguzi kabla ya kukamata watu kiholela.

“Hawa vijana wapo na ni vijana ambao wamekosa mwelekeo. Hata hivyo, idara husika zinafaa kuchunguza kwanini wanajihusisha na mambo hayo. Kukamata watu ovyo ovyo sio suluhisho,” alisema Mwarandu, mmoja wa wazee hao.

Aidha, wazee hao walisema kuwa vijana wengi wamekosa elimu ya kutosha, jambo linalowafanya kujihusisha na vitendo vya uhalifu bila kufikiria maisha yao ya badae.

Kauli hii inakuja huku wanaharakati katikaeneo la Msambweni wakitahatharisha vijana dhidi ya ushawishi wa kujiunga na kundi la MRC.

Suleiman Kuwasha, mwanaharakati wa kijamii, aliwasihi vijana wa eneo hilo la Pwani kujisajili kupata vitambulisho vya kitaifa na kuwaonya dhidi ya kuendeleza shughuli za kuindi hilo.

“Ni kweli vuguvugu la MRC lipo lakini wakati wa kuingilia maswala hayo haujafika. Vijana tuangalie mambo ya maendeleo ya taifa,” alisema Kuwasha.

Kundi la MRC liligonga vichwa vya habari humu nchini miaka kadhaa iliyopita baada ya kuanzisha mchakato wa kutenga eneo la Pwani kama sehemu inayojisimamia, kabla serikali kukabiliana nalo la kuliharamisha.