Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wazee kutoka shamba la Banita lililo eneo bunge la Rongai wamekubali kusitisha mapigano na mgogoro uliyokumba shamba hilo kwa muda mrefu.

Wazee hao wakiwakilisha jamii ya pande tatu ambao ni Joseph Kamau Wainaina, Patrick Chepkurgur, pamoja na mwakilishi wa jamii za wachache kasisi Leonard Amboka, walikubali kusuluhisha mzozo wa shamba hilo lenye ekari elfu 14 kwa njia mbadala ya mazungumzo, badala ya kukimbilia mahakamani.

Huku mkutano huo uliohusisha mbunge wa eneo bunge hilo Raymond Moi, mkuu wa tume ya ardhi ya kaunti ya Nakuru Frank Kimbelekenya, Mwenyekiti wa bodi ya usimamizi wa ardhi kaunti ya nakuru Victor Prengei, wazee hao walipendekeza kuhusishwa kwa wanaume, wanawake, vijana na hata wazee katika michezo mbalimbali huku wakingiojea ripoti kutoka kwa kamati ya bunge kuhusu ardhi itakayotoa tathmini ya walengwa wa shamba hilo, na kiwango cha ardhi ambacho kila mmoja wa ardhi hiyo anafaa kupewa.

Hatua hii inafuatia ushirikishi wa mwenyekiti wa bodi ya usimamizi wa ardhi katika Kaunti ya Nakuru Victor Pregei ambaye amekuwa akiwaelekeza kutumia mbinu mbadala ya mazungumzo pasi na kwenda mahakama au hata kutumia nguvu za polisi, jambo ambalo amesema huchukua muda mwingi na pia ghali.

Hata hivyo, wazee hao wakizungumza katika kikao jumanne wiki hii kilichoandaliwa na shirika la IDPAC Kenya chini ya mwenyekiti wake Kepha Magenyi walikubaliana ya kwamba hakuna mwanasiasa mwenye nia mbaya atakayewagonganisha.