Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyibiashara wa soko la Daraja mbili mjini kisii wamemtaka waziri wa biashara katika Kaunti ya Kisii Kebati Osoro kueleza jinsi millioni 3.8 zilitumika kukarabati soko hilo.

Hii ni baada ya waziri huyo kutoa ripoti mapema wiki hii kuwa serikali ya kaunti hiyo ilitumia shillingi millioni 3.8 kukarabati soko hilo, jambo ambalo wafanyibiashara wa soko hilo wamelikosoa vikali na kusema ni kudanganya wakazi kwani hakuna chochote kimefanywa.

Sasa waziri Kebati ametakiwa kueleza jinsi pesa hizo zilitumika na kazi ipi zilifanya katika soko hilo ili kuonyesha uwazi wa utumizi wa fedha za serikali.

Wakizungumza siku ya Alhamisi katika soko la Daraja Mbili mjini Kisii, wafanyibiashara hao, wakiongozwa na Elijah Michieka na Mary Obara walimkosoa waziri huyo kwa kutoa habari ambayo isiyokuwa ya ukweli, huku wakitaka waziri huyo kujitokeza bayana na kueleza jinsi pesa hizo zilitumika kulingana na ripoti aliyotoa mapema wiki hii.

“Serikali ya Kaunti ya Kisii imekuwa ikidanganya kuwa itakarabati soko hili la Daraja Mbili kwa muda mrefu sasa na haijafanya chochote,” alisema Elijah Michiweka

“Mapema wiki hii waziri wa biashara Kebati Osoro alisikika kwa kutoa habari kuwa serikali ya kaunti imetumia millioni 3.8 kukarabati soko hili na hakuna chochote kimefanywa,  tunataka waziri huyo ajitokeze aeleze jinsi pesa hizo zimetumika,” aliongeza Michieka.

Kwa upande wa waziri huyo Osoro alisema alisikika vibaya, na kusema pesa hizo zilitumika kutengeneza kivukio kilichoko katika soko hilo na kutengeneza mahali magari yanaegezwa katika soko hilo la Daraja Mbili.