Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Waziri wa biashara, utalii na vyama vya ushirika katika Kaunti ya Nyamira John Omanwa amewaomba wanabiashara katika kaunti hiyo kuhakikisha kuwa wamejisajili kupata leseni mpya za kuhudumu. 

Akihutubia wanabiashara hao mjini Nyamira siku ya Jumatano, Omanwa alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wanabiashara wanajisajili kupata leseni za kuhudumu kwenye mtandao ili kuwaruhusu kupata huduma hizo kwa haraka pasina kulazimika kupanga foleni kwenye afisi za wizara hiyo ili kupokezwa leseni. 

"Tumeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wanabiashara wanaweza kulipa na kujisajili kupata leseni za kuhudumu kupitia kwenye mtandao ili kupunguza mda unaotumika na wanabiashara hao kupanga foleni katika afisi za wizara ili kupata leseni hizo," alisema Omanwa. 

Omanwa aidha aliongeza kuwa hatua hiyo itaisaidia pakubwa wizara yake kuangamiza visa vya ufisadi, huku akiwaonya vikali wanabiashara walio na mazoea ya kutosajili biashara zao kupata leseni zakuhudumu. 

"Hakika hatua hii ya wanabiashara kusajili biashara zao kwa njia ya mtandao itatusaidia pakubwa sisi kama wizara kupambana na visa vya ufisadi ambavyo vimekuwa vikisababisha wizara hii kupoteza mamillioni ya pesa, ila pia ni onyo kwa wanabiashara ambao wana mazoea ya kukwepa kusajili biashara zao na yeyote atakayepatikana na hatia hiyo atachukuliwa hatua kali," alihoji Omanwa. 

Waziri omanwa alihaidi kuwa huduma hizo za kupata leseni zitakuwa kwenye mtandao kabla ya mwisho wa wiki hii.