Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaisery ametoa onyo dhidi ya watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kuujumu usalama wa kitaifa.

Waziri huyo amesema kuwa idara ya usalama nchini inafuatilia kwa makini baadhi ya watu wanaosambaza jumbe pamoja na picha zinazohusiana na shambulizi la Ijumaa la Al Shabab dhidi ya jeshi la KDF nchini Somalia.

Akiongea katika kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi, waziri huyo alisema kuwa hatua hiyo inachangia kuwapa nguvu magaidi.

Hatua hii inatokana na tetesi kwamba kuna picha zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zinazohusishwa na shambulizi hilo bila idhini kutoka kwa idara ya usalama.

Kila siku teknolojia inaendelea kukua huku mitandao mbalimbali ya kijamii ikibuniwa kama njia moja ya kurahisisha mawasiliano, na hiyo inatoa fursa kwa watu kusambaza jumbe au picha za aina yoyote kwa haraka zaidi.

Siku ya Ijumaa, magaidi wa Al Shabab wanadaiwa kuvamia kambi ya jeshi la AMISOM eneo la El Adde nchini Somalia, ambapo wanajeshi kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Wakati wa kikao hicho hata hivyo, waziri Nkaisery alidinda kueleza idadi kamili ya wanajeshi waliouawa katika shambulizi hilo akisema kuwa serikali itatoa takwimu hizo baadae.