Spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki na wawakilishi wadi wa kaunti hiyo wameagiza waziri wa fedha katika kaunti hiyo kufika mbele ya bunge hilo kueleza bayana jinsi pesa za mwaka 2014/2015 zilitumika kufanya miradi ya maendeleo.
Hii ni baada ya ripoti kuonyesha kuwa pesa nyingi zilitumika kukarabati barabara, kujenga mazahanati, maktaba za vitabu, kujenga nyumba ya kifahali ya gavana wa kaunti hiyo James Ongwae, huku mamillioni ya pesa yakitumika kwa njia isiyo na uwazi.
Akizungumza siku ya Jumatano katika vikao vya bunge hilo, mwakilishi wa wadi ya Ichuni Francis Aburi, mwakilishi wa Sengera Timothy Nyarang’o na wengine walisema yaliyoandikiwa kwa ripoti hiyo si ya ukweli, na kusema huo ni ubadhilifu wa pesa.
Aidha, walimtaka waziri wa fedha katika kaunti hiyo Kodek Migiro na maafisa wake kufika mbele ya bunge hilo kueleza jinsi pesa hizo zilitumika, na ni wapi zilitumika ili kueleza ukweli na uwazi.
“Hakuna maktaba ya vitabu imejengwa katika kaunti ya Kisii, hakuna ukarabati wa barabara umekamilika, hakuna zahanati imejengwa, lakini ripoti inaonyesha kuwa mamilioni ya pesa yametumika kwa miradi ambayo hatuoni,” alisema Aburi
“Tunataka kuelezwa pesa hizi zilienda wapi ili wakazi wa kaunti ya Kisii wajue jinsi pesa zao zinatumika,” alisema Nyarang’o.
Spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki alilazimika kuagiza waziri wa fedha na maafisa wake kufika mbele ya bunge la kaunti hiyo kueleza hayo yote.