Share news tips with us here at Hivisasa

Wamiliki wa matatu mjini Nakuru wameonywa dhidi ya kuwaajiri wanafunzi kama manamba wa matatu zao.

Mwenyekiti wa miungano ya matatu mjini Nakuru Stephen Muli amesema kuwa wamegundua baadhi ya wenye magari wamewaajiri vijana waliomaliza kidato cha nee kama makanga.

Muli amesema kuwa hwatakubali vijana wasiokuwa na vitambulisho vya taifa na walio chini ya umri wa miaka 18 kuhudumu kama makanga.

Akiongea mjini Nakuru jumanne,Muli alisema kuwa matatu yeyote itakayo kiuka agizo hilo itapigwa marufuku ya kuhudumu.

“Wakati huu ambapo shule zimefunga kuna baadhi ya vijana wadogo wameajiriwa kama makanga na sisi kama wasimamizi wa matatu mjini Nakuru hatutakubali hilo lifanyike.Tunawaonya wenye magari kuwa wasiwajiri vijana walio chini ya umri wa miaka kumi na nane kwa kuwa hiyo ni kinyume cha sheria,” alisema Muli.

“Iwapo matatu itapatikana na makanga mwanafunzi ama asiye na kitambulisho basi sisi tutaipiga marufuku na haitahudumu Nakuru,” aliongeza.

Aliwataka madereva na makanga wote kudumisha nidhamu ya hali ya juu wakati huu wa msimu wa krismasi na kuheshimu sheria zote za trafiki.

“Kila mwanachama wetu anatakiwa kudumisha nidhamu kazini na kuheshimu abiria pamoja na sheria za barabarani ili tuweze kuepuka maafa wakati huu wa likizo,” alisema.

Aidha Muli aliongeza kuwa watashirikiana na mafias wa polisi kuhakikisha kuwasheria za trafiki zinafuata na wanachama wao wote.