Baada ya zoezi la kuwachunguza wakuu wa idara katika Kaunti ya Kisii kuanza siku ya Jumanne katika bunge la kaunti hiyo ili kueleza jinsi pesa za maendeleo katika bajeti ya mwaka wa 2014/2015 zilivyotumika, tayari wizara moja ya utawala imekosolewa vikali kwa kutumia pesa vibaya.
Hii ni baada ya wizara hiyo ikiongozwa na waziri Peris Onsarigo kutumia zaidi ya milioni ishirini kujenga mahakama ya serikali ya kaunti hiyo na afisi ya wakili wa kaunti kabla ya wawakilishi wadi kujulishwa, kujadili na kupitisha.
Kulingana na waakilishi wadi wa kaunti hiyo, wakiongozwa na mwakilishi wa wadi ya Bokimonge George Bibao, wa Sengera Timothy Nyarang’o ni kuwa hakuna kipengele cha katiba kinachoruhusu utumizi wa pesa za serikali kabla ya wahusika kujulishwa na kupitisha.
Wakizungumza siku ya Jumanne katika bunge hilo mjini Kisii, waakilishi hao walikosoa wizara hiyo kwa kubadhilisha pesa za umma kwa kutumia pesa hizo vibaya.
Ata hivyo, waziri Onsarigo alijitetea vikali kwa kusema mahakama ilijengwa ili mfanyibiashara anaposusia kulipa ushuru apelekwe huko ili kushtakiwa na kulipa ushuru kwani serikali haiwezi kuendelea bila ushuru, jambo ambalo wawakilishi walikataa na kusema wangejulishwa kabla ya kufanya hivyo ili kupitisha
“Jinsi imeonekana, katiba haifuatwi maana pesa za umma hutumika kabla ya wawakilishi wadi kujulishwa na kupitisha, tunaomba uwazi ili pesa za umma zitumike vizuri,” alisema Bibao.
Zoezi hilo la mawaziri kueleza jinsi pesa zilitumika katika wizara zao laendelea.