Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kina mama katika wadi ya Kabatini katika eneo bunge la Bahati wana kila sababu ya kutabasamu baada ya zahanati ya eneo hilo kuanza kutoa huduma za kujifungua kwa kina mama.

Zahanati hiyo ambayo ujenzi wake ulifadhiliwa na serikali ya Kaunti ya Nakuru ilianza kutoa huduma hizo hapo Jumatano bila malipo.

Afisa mkuu wa afya katika zahanati hiyo James Njoroge amesema kuwa kuanzishwa kwa huduma hiyo ni afueni kwa kina mama waliolazimika kusafiri hadi Nakuru mjini au Bahati kutafuta huduma hiyo.

Akizungumza siku ya Jumatano, Njoroge alisema kuwa kina mama watapata huduma zote zinazohusiana na uja uzito bila malipo.

"Tunafurahi kuona kuwa hatimaye kina mama kutoka kabatini na maeneo jirani wataweza kupata huduma ya kujifungua hapa karibu na bila kugharamika," akasema Njoroge.

"Zahanati hii itaweza kuwahudumia kina mama wapatao kumi na tano kwa kila siku na itahudumia wakazi wa hapa kabatini na maeneo jirani," aliongeza.

Kando na kuhudumia kina mama, zahanati hiyo pia itatoa huduma zingine za afya kwa wakaazi wa eneo hilo.

"Tayari tumepata wahudumu wa afya na tuna vifaa vya kutuwezesha kuwahudumia watu wa kabatini," aliongeza afisa huyo.

Aidha Njoroge aliitaka serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa zahanati hiyo inapata ambulansi ili kuiwezesha kutoa huduma za dharura.