Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya magari 30 yalinaswa katika operesheni iliyofanywa na maafisa wa trafiki mjini Mombasa siku ya Jumatatu, kufuatia agizo la halmashauri ya uchukuzi na uslama barabarani NTSA.

Akizungumza na wanahabari wakati wa operesheni hiyo, kaimu afisa mkuu wa trafiki mjini Mombasa, Solomon Njuguna, alisema kuwa magari yaliyokamatwa ni yale yenye vioo ambavyo vimetiwa rangi, magari yenye michoro pamoja na yale yenye muziki wa sauti ya juu.

“Magari mengine yametiwa rangi kimo cha kutoyaona yanayojiri ndani. Afisa wa usalama atajuaje nani amebebwa ndani ama ni nini inasafirishwa? Mambo haya lazima yakomeshwe,” alisema Njuguna.

Afisa huyo aidha aliwaonya madereva wa magari ya uchukuzi kuwa watakabiliwa vikali kwa mjibu wa sheria iwapo watakosa kuzitii sheria mpya za barabara.

Hata hivyo, madereva hao wamezipinga sheria hizo na kuzitaja kama zinazolenga kuwakandamiza vijana wanaoitegemea sekta ya uchukuzi kama ajira.

“Wengi wetu tumeyaacha matumizi ya dawa za kulevya ili kujiunga na biashara ya magari kujikimu kimaisha. Kama sasa hapa pia tunalengwa, tutakwenda wapi,” alisema mmoja wao.

Halmashauri ya uchukuzi na usalama barabarani nchini NTSA ilitangaza siku ya Jumatatu, kama siku ambayo magari ya umma ambayo hayatakua yamefuata sheria mpya za uchukuzi yataondolewa barabarani.