Baadhi ya wanafunzi mayatima na wale wanaotoka katika familia zisizo jiweza katika Kaunti ya Nyamira huenda wakafaidikia pakubwa kutokana na mradi wa benki ya Equity kufadhili elimu ya watoto werevu kwenye shule za upili.
Kulingana na meneja wa benki ya Equity tawi la Nyamira Edward Ombiro, tawi hilo linapania kuwafadhili zaidi ya wanafunzi hamsini waliopata alama 350 na zaidi, kwenye mtihani wa kitaifa wa shule ya msingi KCPE.
Ombiro alisema kuwa watakaopewa kipau mbele ni watoto mayatima.
"Zaidi ya wanafunzi 400 walituma maombi ya kutaka kupata ufadhili wa masomo almaarufu 'Wings to Fly', ila tulichuja idadi hiyo hadi wakasalia 100. Tutahakikisha kuwa wanafunzi waliohitimu na hasa mayatima wananufaika kutokana na mpango huu," alisema Ombiro.
Ombiro aliwaonya wazazi na walezi walio na mazoea ya kupeana ripoti za uongo ili watoto wao wanufaike kutokana na mpango huo, huku akiongezea kuwa azimio la benki hiyo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wamepata elimu itakayo wafaa siku zao za usoni.
"Kuna wazazi na hata walezi walio na mazoea ya kupeana ripoti za uongo kuhusiana na wanafunzi fulani ili kutupumbaza kuwa wanafunzi husika wanahitaji msaada. Ningependa kuwaonya kwasababu yeyote atakaye patikana atachukuliwa hatua kali za kisheria. Nia yetu sisi ni kuwawezesha wanafunzi wasiojiweza kupata elimu itakayo wafaa maishani," aliongezea Ombiro.