Michezo ya kuigiza na mziki katika kiwango cha shule za msingi kwenye wilaya ya Kisii ya Kati, katika kaunti ya Kisii, zimeanza hii leo Jumatu, ambapo wanafunzi kutoka shule mbali mbali wamejitoma kushindana kwenye viwango tofauti tofauti.
Kulingana na mwenyekiti wa mashindano hayo Bwa Nahashon Ooga, kutakuwa na vitengo vya nyimbo za kiafrika yaani ‘African folk song’, mashairi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza, uimbaji wa nyimbo zilizopendwa miongoni mwa vitengo vingine.
Bwana Ooga alisema kuwa mashindano hayo yanaendelea kwa siku mbili, na kuahidi kuwa watajitahidi kuwapa wanafunzi wanaoshiriki msaada unaofaa ili waweze kunoa makali katika talanta zao za kuigiza, kughani mashairi na kuimba.
Aliomba serikali ya Kisii kuhakikisha kuwa wanawapa msaada kifedha na kuwajengea ukumbi mahususi wa kufanyia mashindano ya talanta za wanafunzi kama njia moja ya kuunga mkono vipaji kwa watoto, kuliko kutumia madarasa ya shule andalizi.
Mwandalizi huyo pia aliwataka wanafunzi wanaoshiriki kuwa na nidhamu na kujiepusha kutoka kuenda mtaani kutembea, na pia kuwasihi walimu wote wanaowakilisha shule zinazoshiriki kuwaangalia watoto wao hadi mwisho wa mashindano hayo.
Tamasha hizo zinaandaliwa katika shule ya msingi ya Kisii, na miongoni mwa shule zinazoshiriki ni kama Shule ya Msingi Jogoo, Nyambera, Shule ya msingi ya Kisii Campus na nyinginezo zinazowakilisha wiyana ya Kisii ya Kati.