Naibu wa chifu wa lokesheni ya Mwamonari, wadi ya Sensi, amewaomba wazee wa vijiji kuwaelimisha wakazi kuhusu umuhimu wa mradi wa Nyumba Kumi.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wengi wa wakazi katika vijiji mbalimbali katika wadi ya Sensi hawajui wema wa mradi huo.
Akizungumza na mwandishi huyu wa habari siku ya Jumatano afisini mwake iliyoko eneo la Masakwe, Nelson Atandi aliomba wazee wa vijiji kujaribu kila wawezalo kuwaelimisha wakazi kuhusu umuhimu wa Nyumba kumi kama njia moja ya kupunguza uhalifu kutekelezwa vijijini kila mara.
“Ikiwa kila mtu katika vijiji vyote vya eneo hili amejua umuhimu na kuelewa mradi wa Nyumba kumi, hatutakuwa na mambo ya uhalifu katika eneo hili kamwe,” alisema Atandi.
Atandi alisema kujua na kufahamu mradi huo ni mojawapo ya kujua malengo ya serikali iliyo nayo ya kupunguza visa vya ujambazi na kuvimaliza pamoja na kuhakikisha kila jirani amemjua jirani yake na mienendo yake.
Naibu huyo wa chifu pia aliwatahadharisha watu ambao wanawaajiri yaya wa nyumba huku akiwaomba kuwachunguza kabla ya kuwapa kazi ili ajira ya yaya isiwe inaleta utatanishi katika nyumba fulani.
Alisema yeyote anayehitaji kupewa ajira ya uyaya ni muhimu kupokezwa barua kutoka kwa chifu ili kubaini anatoka sehemu ipi.
Haya yanajiri baada ya visa vya wizi kuongezeka katika eneo hilo, jambo ambalo liliwalazimu machifu na manaibu wao kutafuta mbinu ya kuvipunguza.