Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Walimu wakuu katika shule za msingi na za upili wameombwa kuwashauri walimu ambao wameathirika kwa matumizi ya dawa za kulevya badala ya kuwaachisha kazi kwani matumizi ya dawa na pombe ni kama ugonjwa mwingine ule.

Akiongea katika mji wa Nyamira siku ya Jumapili, Naibu katibu mkuu wa Chama cha walimu wa shule za upili na taasisi (KUPPET) Julias Korir, alisema kuwa walimu wakuu wamekuwa na mtindo wa kuwasimamisha kazi baadhi ya walimu ambao wana tabia ya kunywa pombe na kulewa kinyume na sheria hali ambayo afisa huyo alitaja kuwa dhuluma kwa waathiria hao.

Bwana Korir alishauri kuwa badala ya kuwanyanyasa wahusika, ni vizuri walimu hao kupelekwa katika vituo vya kuimarisha na kurekebisha tabia zao na kurejelea hali yao ya kawaida ya kuwafundisha wanafunzi, kwani ulevi ni ugonjwa tu kama magonjwa mengine.

Aidha, afisa huyo wa walimu alishangaa ni vipi walimu hao husimamishwa kazi ilhali masomo ambayo wanafunza mara nyingi ndio wanafunzi hupita vizuri. Aliwasihi walimu wote kushikana mikono kuendeleza elimu na kutafuta njia mbadala ya kuwaadhibu walimu husika.

"Walimu wengi ambao ni walevi hufanya bora katika vitengo ambavyo hua wanasomesha, kwa hiyo sio vizuri kuwafuta kazi walimu kama hao, nawaomba wakuu wa shule ambazo zinakuwa na walimu walevi kuwapeleka walimu hao katika vituo vya kuimarisha na kurekebisha uraibu huo ili nao waweze kukaa kama wengine," alisihi Korir.